Wednesday, January 20, 2016

Makusanyo ya halmashauri yaongezeka kwa 800%.

MAKUSANYO ya mapato katika halmashauri nchini, yameongezeka kufikia asilimia 800 hadi 900 baada ya kuanza kutumika kwa mfumo wa kukusanya mapato kwa njia ya kielektroniki katika halmashauri 164.
Hayo yalibainishwa jana na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jaffo wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari mjini hapa.
Jaffo alisema Serikali imesanifu na kutengeneza mfumo wa kukusanya na kutoa ankara na hati za madai kwa kodi na tozo mbalimbali katika mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuachana na utaratibu wa kukusanya mapato kwa kutumia hati zinazoandikwa kwa mkono.
Alisema tangu halmashauri kuanza kutumia mfumo wa kukusanya mapato kwa njia ya kieletroniki, makusanyo yameongezeka kwa asilimia 800 hadi 900, hali ambayo inadhihirisha ukusanyaji mapato kwa njia ya stakabadhi za kuandikwa kwa mikono fedha nyingi zilikuwa zikipotea.
Alisema msingi wa kuanzishwa kwa matumizi ya mfumo huo ni kuanzisha matumizi ya benki ya TEHAMA katika kukusanya kodi na tozo mbalimbali na kuachana na utaratibu wa kukusanya mapato hayo kwa kutumia stakabadhi za kuandikwa kwa mkono, ambao hutengeneza mianya ya wizi na ubadhirifu wa fedha.
Alisema mfumo huo umekusudia kurahisisha utoaji wa stakabadhi na utunzaji kumbukumbu na kudhibiti upotevu wa mapato katika vyombo vinavyokusanya fedha za umma. Alisema serikali iliagiza ifikapo Ju.lai 1, 2015, halmashauri zote ziwe zimeanza matumizi ya ukusanyaji wa mapato kwa mfumo wa kielektroniki, lakini ilipofika tarehe hiyo halmashauri 51 sawa na asilimia 28.18 ya halmashauri zote nchini, ndizo zilikuwa zimetekeleza agizo hilo.
Aidha, hadi mwanzoni mwa Desemba 2015 ni halmashauri 86 pekee sawa na asilimia 47.78 ndizo zilikuwa zimeingia katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa agizo la serikali licha ya kupewa muda hadi Desemba 31, 2015.
Alisema kutokana na kusuasua kwa zoezi hilo la serikali, ndipo agizo la msisitizo lilitolewa na Ofisi ya Rais Tamisemi kuwa ifikapo Januari 10, mwaka huu halmashauri zote ziwe zimeingia katika mfumo huo; hivyo hadi Januari 12, halmashauri 164 sawa na asilimia 90.6 zimeingia katika hatua mbalimbali za ufungaji na matumizi ya mfumo.
Pia halmashauri 17 mpya sawa na asilimia 9.4, hazijaanza mchakato wa kufunga mfumo kwa sababu mbalimbali, zikiwemo kutokuwa na ofisi ya kudumu, kutofikiwa na Mkongo wa Taifa, umeme na zingine hazijagawana mali na halmashauri mama. Alizitaka zijipange kufunga mfumo huo

KIVUTIO CHA UTALII MKOANI SONGWE.



Image result for mbozi meteorite
Kimondo cha Mbozi ni kimondo ambacho kimeanguka kutoka angani karibu na mji wa Vwawa. Kinakadiriwa kuwa na uzito wa zaidi ya tani 12, kilianguka katika kilima cha Mlenje, wilayani Mbozi katika mkoa wa Mbeya, Tanzania.
Kipo kati ya vimondo vizito 10 vinavyojulikana duniani. Kina urefu wa mita 3.3, upana wa mita 1.63 na kimo cha mita 1.22.
Kina maumbile maalum tofauti na vimondo vingine vinavyopatikana ulimwenguni kwa kuwa hiki ni hasa cha chuma .Wadau wa mkoa wa Songwe wanapenda kuwakaribisha kutembelea eneo hilo.

Serikali Yakanusha Uzushi Unaoenezwa Katika Mitandao ya Kijamii Kumhusu Rais Magufuli .

Hivi karibuni kumejitokeza uzushi unaosambazwa katika mitandao ya kijamii ya ndani ya nchi na nje ya nchi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli amefukuza wageni kutoka nje  waliokuwa wanafanyabiashara zao nchini kwa kuwa serikali yake haitaki wageni kufanya biashara nchini.

Serikali haijafukuza wageni kutoka nje ya nchi kufanya biashara nchini na haina mpango wa kuwafukuza wageni wanaoishi nchini kwa vibali vilivyotolewa kisheria na Idara ya Uhamiaji.

Uzushi huo usiokuwa na ukweli umeenezwa kufuatia Idara ya Uhamiaji kutekeleza jukumu lake la kufuatilia wageni wote wanaoishi nchini bila vibali halali vya ukaazi ambapo kwa mwezi Novemba na Desemba mwaka 2015 wageni 372 walioondoshwa nchini.

Kazi ya kufuatilia wageni wanaoishi nchini bila vibali halali vya kisheria haijaanza katika Serikali ya Awamu ya Tano. Idara ya Uhamiaji nchini tangu Januari hadi Desemba mwaka jana iliondosha nchini jumla ya wageni 1,642 waliokuwa wanaishi na kufanya shughuli zao nchini kinyume na Sheria.

Uzushi unaoenezwa hauna ukweli wowote na hauna nia njema na nchi yetu kwani kati ya mwaka 2014 na 2016 Idara ya Uhamiaji imetoa vibali vya ukaazi  (Residence Permits) 40,765 kwa wageni wawekezaji na wafanyabiashara, wageni wanaofanyakazi za kuajiriwa, wageni wanaokuja kwa ajili ya Masomo, matibabu, dini, utafiti na wastaafu kuishi na kufanya shughuli zao nchini.

Serikali inawakaribisha wageni kuja nchini kuwekeza na kufanya shughuli zao kwa kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu za nchi.

Aidha, kuna uzushi unaenezwa kuwa Rais Dkt John Pombe Magufuli amepiga marufuku wanawake kuvaa nguo fupi kama njia ya kupunguza kasi ya maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI.

Mheshimiwa Rais tangu aingie madarakani hajawahi kuagiza wala kutoa tamko kuhusiana na uzushi wa kukataza uvaaji wa nguo fupi ili kupunguza maambukizi ya Ukimwi kama inavyoenezwa katika mitandao ya ndani na Nje ya Nchi  ambayo inanukuu habari hiyo kuwa imeandikwa na Gazeti la Kenya “The Standard”

Serikali inapenda kuutangazia umma kuwa uzushi huo unaomhusu Mheshimiwa Rais Magufuli umetungwa na watu wasioitakia mema nchi yetu kwa lengo la kumdhalilisha Rais na hauna ukweli hivyo watu wasishiriki kuueneza kwa njia yeyote ile.

Serikali kupitia balozi zake za Kenya na Afrika Kusini zinafuatilia chanzo cha uzushi huu kuhusu Rais Magufuli kwa kushirikiana na nchi husika na watakaobainika kutunga na kueneza uzushi huu watachukuliwa hatua za kisheria.