Kutokana na ongezeko la mahitaji ya nishati ya umeme nchini, nishati
itokanayo na jotoardhi imeelezwa kuwa muhimu kwa kuwa itachangia katika
kukidhi mahitaji ya nishati ambayo ni kiunganishi kikuu cha ukuaji wa
uchumi.
Akiwasilisha mada katika Kongamano la Tano la Kimataifa la Jotoardhi
kwa nchi za Bonde la Ufa, lililofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe
27Oktoba – 2 Novemba, 2014, amesema kuwa jotoardhi inaweza kuwa
suluhisho la mahitaji ya nishati kwa Tanzania na dunia.
“Tanzania inahitaji nishati mchanganyiko ikiwemo itokanayo na
jotoardhi ili kukidhi mahitaji ya nishati ya umeme nchini ambayo
mahitaji yake yamekua kwa kiasi cha asilimia 12-15 kwa mwaka mmoja,”
alieleza Mhandisi Mbise.
Kamishna Mbise alifafanua kuwa, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2015
Tanzania itakuwa imeunganishwa na nishati ya umeme unaofikia kiasi cha
megawati 3000 ambapo ifikapo mwaka 2033 kiasi cha megawati za umeme
10,000 zinatarajiwa kuzalishwa.
Alieleza kuwa, zipo fursa kwa sekta binafsi kushiriki katika shughuli
za uwekezaji na uendelezaji wa nishati hiyo kutokana na uwepo wa Sera
mpya ya Nishati ya mwaka 2014 ambayo imezingatia masuala ya nishati
jadidifu ikiwemo jotoardhi, Sheria ya umeme ya mwaka 2008, Sera ya
ushiriki wa sekta ya Umma na Sekta Binafsi ya mwaka 2009 na taratibu
nyinginezo.
Kamishna Mbise alisema kuwa, Serikali itahakikisha kuwa inaendeleza
nishati ya jotoardhi kutokana na mazingira bora yanayoruhusu kuendeleza
nishati hiyo ikiwemo kuanzishwa kwa Kampuni ya Maendeleo ya Jotoardhi ya
Taifa (TGDC), mchango wa serikali katika kusaidia masuala ya
uchorongaji katika maeneo ya Ziwa Ngozi na Songwe Mkoani Mbeya, katika
Ziwa Natron (Manyara), Kisaki Morogoro na Luhoi (Pwani).
Aidha, Kamishna Mbise alisema kuwa, taasisi za Kimataifa zimetoa
kipaumbele cha kuendeleza jotoardhi Tanzania na Afrika zikiwemo Benki ya
Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Shirika la Umoja wa
Maendeleo la Japani (JICA), Shirika la Kimataifa linaloshughulikia
Mazingira (UNEP) na Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID).
Ameongeza kuwa ushirikiano huo na mazingira wezeshi yataiwezesha
Tanzania kufikia lengo la kuzalisha megawati 200 zitakazotokana na
jotoardhi ifikapo mwaka, 2020.
Imeandaliwa na:
Asteria Muhozya,
Afisa Habari,
Wizara ya Nishati na Madini,
754/33 Mtaa wa Samora,
S.L.P 2000 Dar es Salaam,
Simu: +255-22-2121606/7, Nukushi: +255-22-2121606
Barua Pepe: info@mem.go.tz
Tovuti: www.mem.go.tz

No comments:
Post a Comment